BODI YA MAJI BONDE LA ZIWA VICTORIA YAANZA ZOEZI LA UCHIMBAJI WA VISIMA 10 KUBORESHA HUDUMA YA MAJI MWANZA
Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria imeanza zoezi la uchimbaji wa visima 10 vya maji katika Wilaya za Ilemela na Nyamagana, litakaloambatana na ujenzi wa miundombinu ya matenki na mabomba ya kusambaza maji kwa wananchi, ikiwa ni kupunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.
Akizungumza wakati wa kukagua zoezi la uchimbaji wa kisima cha kwanza katika Mtaa wa Ibinza, Kata ya Nyamhongolo, Wilaya ya Ilemela, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe. Amir Mkalipa, ameishukuru Serikali kwa kuidhinisha Shilingi milioni 500 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, ambao unatarajiwa kunufaisha wakazi wa mitaa ya Ibinza, Iwelyashinga na Nyamhongolo pamoja na maeneo ya jirani. Aidha, amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kuruhusu maeneo yao kutumika kwa uchimbaji wa visima na ujenzi wa miundombinu ya maji.
Mhe. Mkalipa ameongeza kuwa vipimo vya awali vinaonesha kuwa maji kutoka kisima hicho yanafaa kwa matumizi ya binadamu, huku matarajio yakiwa ni huduma hiyo kuanza kuwafikia wananchi ndani ya mwezi mmoja.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, Dkt. Renatus Shinhu, amesema Bodi imeanza kutekeleza maelekezo ya Waziri wa Maji na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji kuhusu uchimbaji wa visima ili kuboresha huduma ya maji kwa wananchi.
Dkt. Shinhu amesema kisima cha kwanza tayari kimefikia kina cha mita 120 na kinatarajiwa kuwa na uwezo wa kutoa lita za ujazo 7,000 za maji kwa saa, hali itakayosaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji katika eneo hilo.
Ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha za utekelezaji wa mradi huo na kuwapongeza viongozi wa Serikali za mitaa pamoja na Diwani wa Kata ya Nyamhongolo kwa ushirikiano wao katika kubaini maeneo yanayofaa kwa uchimbaji. Amesema tathmini katika maeneo mengine pia imeonesha uwepo wa maji na kwamba hatua za utekelezaji zinaendelea.
Nae Diwani wa Kata ya Nyamhongolo, Mhe. Safia Mkama Mzee, ameishukuru Serikali kwa kuanza kutekeleza mradi huo, akieleza kuwa utasaidia kupunguza adha ya upatikanaji wa maji kwa wananchi. Pia, amewataka wananchi kutunza miundombinu itakayojengwa na kuwashukuru waliojitolea maeneo yao kwa ajili ya uchimbaji wa visima na ujenzi wa matenki.