BODI YA MAJI BONDE LA ZIWA VICTORIA YAFANYA UTAFITI WA MAJI CHINI YA ARDHI KATIKA KATA YA KAYENZE, MANISPAA YA ILEMELA
Timu ya wataalamu kutoka Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria imefanya zoezi la utafiti wa maji chini ya ardhi katika Kata ya Kayenze, Manispaa ya Ilemela, Mkoa wa Mwanza, ukihusisha mitaa ya Lutongo, Iseni na Iponyabugali.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mhaidrojiolojia wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, Bw. Edsonsweet Protase Deusdedit, amesema kuwa mitaa hiyo ni miongoni mwa mitaa 22 iliyopangiwa kufanyiwa utafiti wa maji chini ya ardhi na kuchimbiwa visima virefu, kwa lengo la kusogeza huduma ya maji karibu na wananchi ndani ya umbali wa mita 400, kwa mujibu wa maelekezo ya Wizara ya Maji.
Utafiti huo umepokelewa vizuri na wananchi wa mitaa hiyo, ambao wameipongeza Bodi kwa kuendelea kufanya tafiti za rasilimali za maji, wakieleza kuwa, hatua hiyo ni muhimu katika kuwezesha upatikanaji wa maji safi na salama na kupunguza adha wanayopata katika kutafuta huduma hiyo.
Zoezi hili ni sehemu ya juhudi za kuimarisha upatikanaji wa rasilimali za maji chini ya ardhi, kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi, pamoja na kupunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi.
Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria inaendelea kutekeleza jukumu lake la kusimamia na kuendeleza rasilimali za maji kwa manufaa ya wananchi na maendeleo endelevu.
ZIWA LETU | UCHUMI WETU | TULITUNZE