Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Maji

Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria

BODI YA MAJI BONDE LA ZIWA VICTORIA YARIDHISHWA NA HATUA ZA UFUNGAJI WA MGODI WA BUZWAGI

Imewekwa: 27 October, 2026
BODI YA MAJI BONDE LA ZIWA VICTORIA YARIDHISHWA NA HATUA ZA UFUNGAJI WA MGODI WA BUZWAGI

Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) imeridhishwa na hatua zinazochukuliwa katika shughuli za ufungaji wa Mgodi wa Buzwagi (Mine Closure), huku kazi hizo zikitarajiwa kukamilika ifikapo Machi 2027.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, Dkt. Renatus Shinhu, wakati wa ziara ya kikazi katika Mgodi wa Buzwagi uliopo Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga, akiwa ameambatana na timu ya wataalamu kutoka Bodi hiyo kwa ajili ya kukagua hatua mbalimbali za kisheria na kiutendaji zinazochukuliwa katika mchakato wa ufungaji wa mgodi.

Katika ziara hiyo, timu ilitembelea maeneo mbalimbali ya mgodi, ikiwemo Tailings Storage Facility (TSF) lililotumika kuhifadhi tope la mabaki ya shughuli za uchimbaji madini, pamoja na shimo la zamani la uchimbaji dhahabu ambalo kwa sasa linatumika kama Pit Lake, yaani eneo linalohifadhi maji ya mvua.

Aidha, timu ilikagua maeneo ya uvunaji na uhifadhi wa maji ya mvua, pamoja na maeneo yanayohusiana na vibali vya matumizi ya maji vilivyotolewa na Bodi. Pia ilikagua eneo lililokuwa limeombewa kibali cha kutiririsha majitaka, ambapo shughuli hizo zimesimama kufuatia kufungwa kwa bwawa lililokuwa likihifadhi tope la mabaki ya uchimbaji madini.

“Kwa ufupi, tumeona shughuli za ufungaji wa Mgodi wa Buzwagi zinaendelea vizuri. Tumekagua maeneo yanayohusiana na matumizi ya maji pamoja na yale yaliyohusiana na majitaka, na tumeridhishwa na hatua zilizochukuliwa, ikiwemo kufungwa kwa bwawa lililokuwa linahifadhi tope la mabaki ya uchimbaji madini,” amesema Dkt. Shinhu.

Ameongeza kuwa mgodi unaendelea na shughuli za urejeshaji wa mazingira, ikiwemo uoteshaji wa miti katika maeneo yaliyotumika kwa shughuli za uchimbaji madini, hatua inayolenga kurejesha mazingira na kuhakikisha maeneo hayo yanakuwa salama na endelevu.

Kwa upande wake, Meneja wa Mgodi wa Buzwagi, Mhandisi Zonnastraal Mumbi, amesema utekelezaji wa mpango wa ufungaji wa mgodi unaendelea vizuri na kwamba shughuli zote zinatarajiwa kukamilika ifikapo Machi 2027.

Ameeleza kuwa hatua zinazotekelezwa katika kipindi hiki zinalenga kuhakikisha maeneo yaliyotumika kwa shughuli za uchimbaji yanarejeshwa na kuwa katika hali salama na endelevu baada ya kukamilika kwa shughuli za uzalishaji.