Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Maji

Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria

WAJUMBE WA BODI YA MAJI BONDE LA ZIWA VICTORIA WATEMBELEA BWAWA LA MANCHIRA KUTATHMINI HALI YA UHIFADHI WAKE

Imewekwa: 05 November, 2026
WAJUMBE WA BODI YA MAJI BONDE LA ZIWA VICTORIA WATEMBELEA BWAWA LA MANCHIRA KUTATHMINI HALI YA UHIFADHI WAKE


Mwenyekiti wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria Bw. Emmanuel Lugomela amewaongoza wajumbe wa Bodi hiyo kutembelea Bwawa la Manchira lililopo Mugumu, Wilaya ya Serengeti, Mkoa wa Mara, kwa lengo la kujionea hali ya uhifadhi wa chanzo hicho muhimu cha maji, changamoto zinazokikabili pamoja na hatua zinazopaswa kuchukuliwa katika kulinda na kuhifadhi bwawa hilo

Akitoa taarifa wakati wa ziara hiyo, Afisa wa Dakio la Mara, Bw. Mwita Mataro, amesema Bwawa la Manchira ni chanzo pekee cha maji kinachohudumia Mji wa Mugumu na vijiji jirani, ambapo kupitia mradi wa uboreshaji wa huduma ya maji unaoendelea, chanzo hicho kinatarajiwa kuhudumia wakazi wapatao 169,000.

Ameeleza kuwa pamoja na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Bodi katika kuhifadhi bwawa hilo, zikiwemo kutenga eneo la hifadhi, kusimika vigingi, kuweka mabango ya makatazo, kufanya doria na kutoa elimu kwa jamii, bado kuna changamoto za uvamizi wa mifugo, ukataji wa miti, uchomaji moto, ongezeko la magugu maji na udongo unaoingia bwawani.

Akizungumza baada ya kutembelea bwawa hilo, Mwenyekiti wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, Bw. Emmanuel Lugomela, amesema suala la Bwawa la Manchira limekuwa likijadiliwa katika vikao vya Bodi kwa muda mrefu, hivyo ziara hiyo imekuwa muhimu katika kuwawezesha wajumbe kujionea hali halisi na kupata uelewa mpana wa changamoto zilizopo.

Amesema taarifa iliyowasilishwa na Ofisi ya Dakio la Mara pamoja na mambo waliyojionea wakati wa ziara hiyo vitasaidia katika majadiliano ya vikao vya Bodi ili kufikia maamuzi yatakayosaidia kulinda na kuendeleza chanzo hicho.

Aidha, Bw. Lugomela amesisitiza umuhimu wa kuzingatia mahitaji ya wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguka bwawa hilo, hususan wafugaji ambao kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa wanategemea chanzo hicho kupata maji ya mifugo yao kutokana na kukosekana kwa vyanzo vingine mbadala.

Ameeleza kuwa pendekezo la kujenga mabirika ya kunyweshea mifugo nje ya eneo la hifadhi ni jambo la msingi linalopaswa kufanyiwa kazi ili kuweka uwiano kati ya mahitaji ya wananchi na wajibu wa kulinda chanzo cha maji.