Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Maji

Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria

BODI YA MAJI YA TAIFA YAFURAHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA LVBWB

Imewekwa: 27 October, 2026
BODI YA MAJI YA TAIFA YAFURAHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA LVBWB

Bodi ya Maji ya Taifa imeipongeza Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria kwa kutumia teknolojia za kisasa katika ukusanyaji na ufuatiliaji wa takwimu za mwenendo wa maji, hatua inayochangia usimamizi endelevu wa rasilimali za maji na upangaji wa miradi ya maendeleo nchini.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Maji ya Taifa, Bw. Hussein Ally, wakati wa ziara ya wajumbe wa Bodi hiyo katika Kituo cha Ufuatiliaji wa Mwenendo wa Maji (Hydrometric Station) cha Ziwa Victoria, kwa lengo la kujionea namna Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria inavyokusanya na kutumia takwimu za maji katika kutekeleza majukumu yake.

Bw. Ally amesema takwimu sahihi ni nyenzo muhimu katika usimamizi wa rasilimali za maji, ikiwemo kufahamu mabadiliko ya kina cha maji, kupanga ugawaji wa maji kwa matumizi mbalimbali na kusaidia usanifu wa miradi ya maendeleo. 

amesisitiza umuhimu wa kuendelea kufuatilia mwenendo wa maji na kutoa tahadhari kwa wananchi kuhusu athari zinazoweza kusababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa, ikiwemo mvua kubwa na mafuriko yanayoweza kujitokeza wakati wa msimu wa mvua.

Nae Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, Dkt. Renatus Shinhu, amesema Bonde hilo lina jumla ya vituo 18 vya kiotomatiki vinavyofuatilia mwenendo wa maji katika ziwa, mito na mabwawa. Vituo hivyo hukusanya taarifa zinazosaidia kufahamu mabadiliko ya viwango vya maji na kuwezesha maamuzi sahihi kuhusu usimamizi na ugawaji wa rasilimali hiyo kwa matumizi ya majumbani, shughuli za kiuchumi na mazingira.

Dkt. Shinhu ameongeza kuwa takwimu hizo ni muhimu pia katika usanifu na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo miundombinu ya barabara na majengo, ili kuzingatia taarifa sahihi za hali ya maji katika maeneo husika.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Rasilimali za Maji kutoka Wizara ya Maji, Bi. Rosemary Rwebugisa, amesema wamejionea juhudi zinazofanywa na Bodi hiyo katika kuhakikisha upatikanaji wa takwimu za maji unaendelea hata pale ambapo msimamizi wa kituo hayupo, kupitia mifumo ya kisasa inayowasilisha taarifa moja kwa moja ofisini. Ameeleza kuwa utaratibu huo ni mzuri na unaweza kuigwa na mabonde mengine ili kuboresha upatikanaji wa takwimu sahihi na za uhakika nchini.