BODI YA MAJI BONDE LA ZIWA VICTORIA YASISITIZA USHIRIKIANO KULINDA BONDE LA MTO KAGERA
Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) imesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau katika kulinda na kurejesha mazingira ya Bonde la mto Kagera, kwa lengo la kuhakikisha uendelevu wa Mradi wa kufua Umeme kwa njia ya maporomoko ya Maji wa Rusumo.
Akizungumza wakati wa kufungua Warsha ya Wadau ya Uandaaji wa Programu ya Uhifadhi wa Bonde la mto Kagera, iliyofanyika Hadjens Hotel jijini Mwanza, Mkurugenzi wa Bodi Dkt. Renatus Shinhu ameeleza kuwa afya ya Bonde hilo ni muhimu kwa uendelevu wa mradi wa kufua umeme kwa njia ya maporomoko ya Maji Rusumo unaozalisha megawati 80 za umeme kwa manufaa ya Tanzania, Rwanda na Burundi.
Amesema changamoto za mmomonyoko wa udongo, uharibifu wa misitu, uchafuzi wa vyanzo vya maji na kuenea kwa gugumaji ni tishio kwa ubora wa maji, uwezo wa kuhifadhi maji na ufanisi wa uzalishaji wa umeme.
Aidha, amesema changamoto hizo haziwezi kutatuliwa na taasisi au nchi moja pekee, hivyo kuna umuhimu wa serikali, jamii, wataalamu, washirika wa maendeleo na wadau wengine kushirikiana katika kuandaa na kutekeleza programu jumuishi ya uhifadhi wa Bonde hilo.
Aidha Bodi imepongeza ushirikiano unaoendelea kati yake, Rusumo Power Company Limited (RPCL) na International Union for Conservation of Nature (IUCN), ikieleza kuwa tayari hatua mbalimbali zimechukuliwa, ikiwemo uwekaji wa alama za mipaka ya mita 60 ya hifadhi ya mito, uwekaji wa mabango pamoja na upandaji wa miti ya asili katika maeneo ya Mito Ruvuvu na Akagera wilayani Ngara.
Warsha hiyo ya siku mbili, inayofanyika tarehe 18–19 Agosti 2026, inalenga kuwaunganisha wadau katika kuandaa programu yenye ushahidi, inayozingatia ushirikiano wa nchi mbalimbali na inayowashirikisha wananchi katika kulinda na kurejesha Bonde la mto Kagera kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Akifunga hotuba yake, mkurugenzi wa Bodi amewashukuru RPCL kwa kuendelea kusaidia na kugharamia shughuli za uhifadhi wa Bonde hilo pamoja na IUCN kwa ushirikiano wake wa kitaalamu katika kuandaa warsha hiyo.