Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Maji

Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria

BODI YA MAJI BONDE LA ZIWA VICTORIA YATOA MAFUNZO YA AFYA YA AKILI KWA WATUMISHI WAKE

Imewekwa: 07 August, 2026
BODI YA MAJI BONDE LA ZIWA VICTORIA YATOA MAFUNZO YA AFYA YA AKILI KWA WATUMISHI WAKE

Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, imeendesha mafunzo ya afya ya akili kwa watumishi wake ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ustawi wa afya na kuongeza tija mahali pa kazi.

Mafunzo hayo yaliyowakutanisha watumishi kutoka madakio yote ya Bodi, yamefanyika katika Ofisi Kuu ya Bodi iliyopo jijini Mwanza.

Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Bodi, Dkt. Renatus Shinhu, amesema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Serikali na Bodi wa kuimarisha ustawi wa watumishi kwa kuwajengea uwezo wa kutambua, kuzuia na kukabiliana na changamoto za afya ya akili ili waendelee kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, utulivu na weledi.

Baada ya mafunzo, watumishi walifanya kikao cha robo mwaka ambapo walijadili masuala mbalimbali ya kiutumishi, kupokea taarifa za utekelezaji wa shughuli za Bodi pamoja na taarifa za matumizi na masuala mengine muhimu yanayohusu maendeleo ya taasisi.

Mikutano hiyo ya robo mwaka imeendelea kuwa sehemu ya utamaduni wa Bodi wa kuimarisha mawasiliano ya ndani, ushirikiano miongoni mwa watumishi na ustawi wao, sambamba na kuhakikisha mazingira bora ya kazi kwa ajili ya utoaji wa huduma bora kwa wananchi.