THE LAUNCHING OF ZANZUI AND MWADILA WATER SOURCES CONSERVATION PROJECT IN MASWA DISTRICT

Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Aweso Julai 29, 2022 amezindua miradi miwili ya uhifadhi wa vyanzo vya maji vya Zanzui (New Sola ) na Mwadila vilivyopo Wilaya ya Maswa.

Katika uzinduzi huo Mheshimiwa Aweso aliipongeza Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria kwa kazi kubwa waliyofanya ya kuhifadhi vyanzo hivyo kwa kishirikiana na viongozi wa Wilaya na jamii.

“Usimamizi wa vyanzo vya maji ni shirikishi na hapa Zanzui na Mwadila mmeweza, inawapongeza sana,” alisema Waziri Aweso.

Awali, akitoa taarifa ya miradi hiyo, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, Bwana Renatus Shinhu alisema tayari Bodi imeweka mipaka ya kudumu katika chanzo cha Zanzui na wamesimika vigingi 250 kuzunguka eneo la chanzo hicho, pia kumepandwa miti 20,000.

Mambo mengine yaliyofanyika katika chanzo hicho cha Zanzui ni pamoja na kulipa fidia kwa wananchi 55, kujenga mabirika ya kunyweshea mifugo na uwekaji wa mabango ya Ilani ya uhifadhi wa chanzo.

Mkurugenzi Shinhu alisema faida zilizopatikana baada ya uhifadhi wa chanzo hicho ni pamoja na kuwepo kwa maji ya kutosha hasa wakati wa kiangazi ambapo kwa sasa bwawa lina maji kiasi cha lita za ujazo bilioni 3.2 ambapo matumizi ya maji kwa sasa ni lita za ujazo milioni nane pekee.

Aliongeza kuwa, pamoja na uwepo wa maji ya kutosha, uhifadhi wa chanzo hicho umesaidia kupungua kwa tope hivyo kuipinguzia Mamlaka ya Maji Maswa gharama za kutibu maji.

Kwa upande wa chanzo cha Mwadila, Mkurugenzi Shinhu alisema Bodi imefanya ukarabati mkubwa wa bwawa hilo lilojengwa miaka ya 1930 ambalo lilipasuka mwaka 1999 wakati wa mvua za Elnino na kusababisha wananchi wa vijiji vya Mwadila na Induki kukosa huduma ya maji kwa zaidi ya miaka 10.

Ukarabati huo ulihusisha uongezaji wa kina cha bwawa kutoka mita mbili hadi nane, unyanyuaji wa tuta, uboreshaji wa utoro wa bwawa, uwekaji wa vigingi 25 kuzunguka bwawa na upandaji wa miti.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji nchini, George Lugomela alimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kubali kuzitembelea bodi zote tisa nchi kwa lengo la kuzindua miradi ya uhifadhi wa vyanzo vya maji.

Bodi za Maji za Mabonde nchini zina majukumu ya kufanya tathmini ya hali ya maji, kusimamia matumizi ya maji kwa njia ya vibali na kuzuia na kudhibiti uchafuzi wa vyanzo hivyo.

Updated: 02/08/2022 — 3:56 pm
Privacy Policy | Terms | Copyright © 2018 Lake Victoria Basin Water Board Website Developed By LVBWB