Mara Day 2021

MAADHIMISHO YA SIKU YA MTO MARA 2021

Tarehe 15 Sptemba kila mwaka ni Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mara ambayo hufanyika kwa kupokezana baina ya nchi mbili za Tanzania na Kenya. Maadhimisho hayo yalitokana na uamuzi wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Bonde la Ziwa Victoria uliofanyika tarehe 04 Mei, 2012 Kigali, Rwanda ulioamua kufanyika kwa maadhimisho ya Siku ya Mto Mara (Mara Day) kila mwaka kuanzia mwaka 2012.

 

Kwa mwaka 2021 maadhimisho ya kumi (10) yamepangwa kufanyika Tanzania, Mkoani Mara katika Wilaya ya Tarime, Kata ya Kemambo, Kijiji cha Murito kuanzia tarehe 12-15 Septemba 2021 kauli mbiu ikiwa “TUHIFADHI MTO MARA KWA UTALII NA UCHUMI ENDELEVU”. Tarehe ya maadhimisho inahusiana na uhamaji wa wanyama kutoka Hifadhi ya Serengeti, Tanzania kwenda Maasai Mara, Kenya kwa ajili ya malisho na kuzaliana na baadaye kurudi Serengeti, Tanzania. Bonde la Mto Mara linachangia kuifanya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kuwa moja ya maajabu 7 ya Dunia kutokana na uhamaji huo wa wanyamapori. Umuhimu huu unazilazimu nchi za Tanzania na Kenya kuweka msukumo mkubwa wa kuhifadhi bonde hilo na kuhakikisha linakuwa endelevu.

 

 LENGO LA MAADHIMISHO YA SIKU YA MTO MARA.

 Maadhimisho hayo hufanyika kwa lengo la kutoa msukumo mkubwa wa kuhifadhi Bonde la Mto Mara unaoanzia milima ya Mau nchini Kenya na kuishia Ziwa Victoria upande wa Tanzania na kuendelea kulitangaza na kulifuatilia tukio muhimu la kuhama kwa wanyama katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Maasai Mara nchini Kenya. Uwepo wa Mto Mara huchangia Rasilimali maji kwenye Ziwa Victoria na vilevile, huchangia kuwepo kwa Hifadhi ya Serengeti ambayo ni tegemeo kubwa la Taifa na wananchi jirani na hifadhi kutokana na shughuli za utalii. Kilele cha maadhimisho haya kitakuwa 15/09/2021 Tarime Mjini ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Hamidu Aweso (Mb).

Privacy Policy | Terms | Copyright © 2018 Lake Victoria Basin Water Board Website Developed By LVBWB