Bodi ya maji Bonde la Ziwa Victoria leo Oktoba 11, 2022 imepokea ugeni wa maafisa wa kijeshi kutoka Chuo cha Ukamanda na Unadhimu cha Duluti Arusha kwa ajili ya ziara ya kujifunza shughuli za bodi katika usimamizi wa rasilimali za maji ndani ya bonde.
Maasifa hao wakiongozwa na Brigedia Jenerali Sylvester Ghuliku ni kutoka Tanzania, Rwanda, Misri, Burundi, Jamhuri ya Kidemocrasia ya Congo, Uganda, Nigeria, Malawi, na Kenya, na wamepokelewa na Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, Bwana Renatus Shinhu.
Brigedia Jenerali Sylvester Ghuliku alisema lengo la ziara ya maofisa hao ni kujifunza shughuli za usimamizi wa rasilimali maji ikiwa ndio kiungo kikubwa cha kiuchumi hasa Ziwa Victoria linalotegemewa na nchi nyingi barani Afrika kwa shughuli za kimaendeleo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bodi Bwana Renatus Shinhu alielezea kuhusu hali ya maji, mafanikio yaliyopatika katika usimamizi wa vyanzo vya maji, changamoto pamoja na mipango iliyopo ya kuhakikisha usalama wa maji unakuwepo kwa wananchi na mazingira.
Akitoa wasilisho lake kwa maafisa hao, Bwana Renatus Shinhu alisema katika kulinda na kuendeleza vyanzo vya maji, Bodi imeendelea kufuatilia wingi na ubora wa maji kupitia vituo zaidi ya 100 vilivyojengwa katika vyanzo mbalimbali katika bonde.
Aliongeza kuwa changamoto zinazokabili shughuli za bonde kwenye usimamizi wa rasilimali za maji ni pamoja na shughuli za uchimbaji wa madini usiozingatia sheria, mabadiliko ya tabia nchi na uvamizi wa vyanzo vya maji kwa shughuli mbalimbali za kibinadamu.
